Saturday 8 October 2011

KISWAHILI HAZINETU, AFRIKA MAENDELEO.

KISWAHILI HAZINETU, AFRIKA MAENDELEO.       30th Sept, 2010


1) Kiswahili tukienzi, hakika kwetu ni kipenzi,
Lugha isiyo kishenzi, kwa umma unaokienzi,
Kongwe masimulizi, wafuasi na waenzi,
Kiswahili hazinetu, Afrika maendeleo.

 2) Lugha iliyo shuari, mazungumzo ni mahamri,
Tamutamu ja sukari, kwa wale wenye habari,
Afrika watu majabari,, Nairobi na Harari,
Kiswahili hazinetu, Afrika maendeleo.

3) Iliyokuwa hatari, bepari kwao hatari,
Inabidi tahadhari, Mwafrika kapata siri,
Hivi yeye machachari, mabepari tahadhari,
Kiswahili hazinetu, Afrika maendeleo.

4) Umoja sasa ndo nguvu, Mwafrika kawa mwerevu,
Fuvu hamna upumbavu, elimu kwao I nguvu,
Wasiwasi kwao kovu, mjinga kawa mwerevu,
Kiswahili hazinetu, Afrika maendeleo.

5) Kenya wao Waswahili, Uganda ni Waswahili,
Tanzania Waswahili, Rwanda pia Waswahili,
Mwafrika we hapo upo, Kiswahili sasa kipo,
Kiswahili hazinetu, Afrika maendeleo.

6) Burundi sasa ndo wapo, mejiunga papo hapo,
Waswahili kwao hapo, Ufaransa teke japo,
Mwafrika we hapo upo, Kiswahilisasa kipo,
Kiswahili hazinetu, Afrika maendeleo.

7) Kwao i Pilipili, Kiswahili ya maboyi,
Afrika kwao ni asili, lugha yao ni mayayi,
Uzungu ni yao hali, Ulaya kwao uhayi,
Kiswahili hazinetu, Afrika maendeleo.

 8) Mwacha mila ndiye mtumwa, anakienzi utumwa,
Ustaarabu wa kutumwa, tayari wamechumwa,
Tayari wewe waumwa, wangoja tu kusukumwa,
Kiswahili hazinetu, Afrika maendeleo.

1 comment:

Abdi M. Abdallah said...

Tukienzi Kiswahili kwani kimesheheni tamaduni zetu Waafrika.