Saturday 8 October 2011

FISI SI MLAFI.

FISI SI MLAFI.                                                                   25 Novemba, 2010

1) Nahuzuni mja miye, fisi atuangamiza,
Anatufanya tuliye, maisha tumepoteza,
Na sisi tuangamiye, vilio ametuliza,
Fisi kweli sio mlafi, ni sisi ndio walafi.

2) Ameapa kulipiza, tulio sisi mang’aa,
Hivio hatotusaza, kwa kumuita tamaa,
Maradhi atuongeza, vifo kwetu ndio baa,
Fisi kweli si mlafi, ni sisi ndio walafi.

3) Vipi tutamwua fisi?  Hili ni muhimu swali,
Kwani chanzo chake ni sisi, jua baada ya hili,
Mependekezwa na sisi, ngawa jawabu hatuli,
Fisi kweli si mlafi, ni sisi ndio walafi.

4) Hino miye ninakinza, mja tumia  kondomu,
Jaribuni kujitunza, inatuongeza hamu,
Si asilimia mia, hino kinga ya kondomu,
Fisi kweli si mlafi, ni sisi ndio walafi.

5) Kwa wale wenye mshiko, kuwa kwake mwaminifu,
Kwao wale wenye jiko, jaribu kuwa nadhifu,
Usimfanye mwenzako, mapema awe ni  mfu,
Fisi kweli si  mlafi, ni sisi ndio walafi.

6) Wamesema mashababu, Ukitaka muua nyoka,
Menena hawa mababu, simpige mwili kaka,
Kichwa ndiyo sababu, ya kufa kwake haraka,
Fisi kweli si mlafi, ni sisi ndio walafi.

7) Zingatia hi zaidi, hino rakamu ya tatu,
Sijaribu kukaidi, iepuke ngono katu,
Bashasha nyiku ya Idi, tapata mwana wa mtu,
Fisi kweli si mlafi, ni sisi ndio walafi.

8) Suluhu ilo muruwa, kuizira hino ngono,
Njia badala huwa, ya kutoa joto hino,
Fikira za uchu towa, tapoteza hizo ndoto,
Fisi kweli si mlafi, ni sisi ndio walafi.

9) Maadili tumekosa, ngono ndiyo kwetu ngoma,
Ngono mekuwa haluwa, wanachekechea pia,
Wadogo wakubwa kuwa, pamoja kusherehekea,
Fisi kweli si mlafi, ni sisi ndio walafi.

10) Walio walafi ni sisi, tunamvizia fisi,
Tumekosa sisi hisi, hisi iliyo halisi,
Vyombo vyetu havihisi, wakati tuna harusi,
Fisi kweli si mlafi, ni sisi ndio walafi.

11) Hivyo chunga hicho chombo, asi mpango wa kando,
Kwani mpango wa kando, ndiyo hasa chake chanzo,
Mpango huu ndiyo chambo, ya kukupeleka ng’ambo,
Fisi kweli si mlafi, ni sisi ndiyo walafi.

12) Uaminifu ndo mambo, kwa wale walo wachumba,
Kuepuka ndiyo jambo, bikira epuka dimba,
Kandanda huwa msimbo, ikiwa utaitimba,
Fisi kweli si mlafi, ni sisi ndio walafi.

13) Kuwaza miye nakoma, mwenzangu we tafakari,
Ukimwi tutauchoma, kwani kwetu ni hatari,
Zingatia nilosema, kwa aushi ya fahari,
     Fisi kweli si mlafi, ni sisi ndio walafi.

No comments: