Showing posts with label Shairi Langu. Show all posts
Showing posts with label Shairi Langu. Show all posts

Saturday, 8 October 2011

FISI SI MLAFI.

FISI SI MLAFI.                                                                   25 Novemba, 2010

1) Nahuzuni mja miye, fisi atuangamiza,
Anatufanya tuliye, maisha tumepoteza,
Na sisi tuangamiye, vilio ametuliza,
Fisi kweli sio mlafi, ni sisi ndio walafi.

2) Ameapa kulipiza, tulio sisi mang’aa,
Hivio hatotusaza, kwa kumuita tamaa,
Maradhi atuongeza, vifo kwetu ndio baa,
Fisi kweli si mlafi, ni sisi ndio walafi.

3) Vipi tutamwua fisi?  Hili ni muhimu swali,
Kwani chanzo chake ni sisi, jua baada ya hili,
Mependekezwa na sisi, ngawa jawabu hatuli,
Fisi kweli si mlafi, ni sisi ndio walafi.

4) Hino miye ninakinza, mja tumia  kondomu,
Jaribuni kujitunza, inatuongeza hamu,
Si asilimia mia, hino kinga ya kondomu,
Fisi kweli si mlafi, ni sisi ndio walafi.

5) Kwa wale wenye mshiko, kuwa kwake mwaminifu,
Kwao wale wenye jiko, jaribu kuwa nadhifu,
Usimfanye mwenzako, mapema awe ni  mfu,
Fisi kweli si  mlafi, ni sisi ndio walafi.

6) Wamesema mashababu, Ukitaka muua nyoka,
Menena hawa mababu, simpige mwili kaka,
Kichwa ndiyo sababu, ya kufa kwake haraka,
Fisi kweli si mlafi, ni sisi ndio walafi.

7) Zingatia hi zaidi, hino rakamu ya tatu,
Sijaribu kukaidi, iepuke ngono katu,
Bashasha nyiku ya Idi, tapata mwana wa mtu,
Fisi kweli si mlafi, ni sisi ndio walafi.

8) Suluhu ilo muruwa, kuizira hino ngono,
Njia badala huwa, ya kutoa joto hino,
Fikira za uchu towa, tapoteza hizo ndoto,
Fisi kweli si mlafi, ni sisi ndio walafi.

9) Maadili tumekosa, ngono ndiyo kwetu ngoma,
Ngono mekuwa haluwa, wanachekechea pia,
Wadogo wakubwa kuwa, pamoja kusherehekea,
Fisi kweli si mlafi, ni sisi ndio walafi.

10) Walio walafi ni sisi, tunamvizia fisi,
Tumekosa sisi hisi, hisi iliyo halisi,
Vyombo vyetu havihisi, wakati tuna harusi,
Fisi kweli si mlafi, ni sisi ndio walafi.

11) Hivyo chunga hicho chombo, asi mpango wa kando,
Kwani mpango wa kando, ndiyo hasa chake chanzo,
Mpango huu ndiyo chambo, ya kukupeleka ng’ambo,
Fisi kweli si mlafi, ni sisi ndiyo walafi.

12) Uaminifu ndo mambo, kwa wale walo wachumba,
Kuepuka ndiyo jambo, bikira epuka dimba,
Kandanda huwa msimbo, ikiwa utaitimba,
Fisi kweli si mlafi, ni sisi ndio walafi.

13) Kuwaza miye nakoma, mwenzangu we tafakari,
Ukimwi tutauchoma, kwani kwetu ni hatari,
Zingatia nilosema, kwa aushi ya fahari,
     Fisi kweli si mlafi, ni sisi ndio walafi.


NI YAKO MAISHA.


NI YAKO MAISHA.                                         24th Nov, 2010

1) Maisha yako maisha, usiwe mshika dau,
Maisha yako maisha, kuwa wewe mwenye dau,
Maisha yako maisha, sije ukaisahau,                
Maisha yako maisha, jitose ndani ya dau.

2) Maisha yako maisha, maisha yako mashuwa,
Maisha yako maisha, nahodha ndiwe hasuwa,
Maisha yako maisha, jaribu piga hatuwa,
Maisha yako maisha, fanya hima kukuwa.

3) Maisha yako maisha, rafikizo wanapaa,
Maisha yako maisha, hata nawe unafaa,
Maisha yako maisha, kurudi nyuma kataa,
Maisha yako maisha, tazama mwendo wa saa.

4) Maisha yako maisha, mwendo ni mrefu kabisa,
Maisha yako maisha, mbio anza sasa,
Maisha yako maisha, usiwachwe nyuma hasa,
Maisha yako maisha, maisha ukawa tasa.

 5) Maisha yako maisha, maisha yako ni maua,
Maisha yako maisha, sijaribu kuyaua,
Maisha yako maisha, jitahidi kufufua,
Maisha yako maisha, yahitaji kuyajua.

6) Maisha yako maisha, omba na yatakupisha,
Maisha yako maisha, Mola atayahuisha,
Maisha yako maisha, jaribu kuyaendesha,
Maisha yako maisha, dereva ni wewe kisha.

7) Maisha yako maisha, tamati nimefika,
Maisha yako maisha, nasaha imenitoka,
Maisha yako maisha, dunia yetu hakika,
Maisha yako maisha, jaribu kubidiika.

KISWAHILI HAZINETU, AFRIKA MAENDELEO.

KISWAHILI HAZINETU, AFRIKA MAENDELEO.       30th Sept, 2010


1) Kiswahili tukienzi, hakika kwetu ni kipenzi,
Lugha isiyo kishenzi, kwa umma unaokienzi,
Kongwe masimulizi, wafuasi na waenzi,
Kiswahili hazinetu, Afrika maendeleo.

 2) Lugha iliyo shuari, mazungumzo ni mahamri,
Tamutamu ja sukari, kwa wale wenye habari,
Afrika watu majabari,, Nairobi na Harari,
Kiswahili hazinetu, Afrika maendeleo.

3) Iliyokuwa hatari, bepari kwao hatari,
Inabidi tahadhari, Mwafrika kapata siri,
Hivi yeye machachari, mabepari tahadhari,
Kiswahili hazinetu, Afrika maendeleo.

4) Umoja sasa ndo nguvu, Mwafrika kawa mwerevu,
Fuvu hamna upumbavu, elimu kwao I nguvu,
Wasiwasi kwao kovu, mjinga kawa mwerevu,
Kiswahili hazinetu, Afrika maendeleo.

5) Kenya wao Waswahili, Uganda ni Waswahili,
Tanzania Waswahili, Rwanda pia Waswahili,
Mwafrika we hapo upo, Kiswahili sasa kipo,
Kiswahili hazinetu, Afrika maendeleo.

6) Burundi sasa ndo wapo, mejiunga papo hapo,
Waswahili kwao hapo, Ufaransa teke japo,
Mwafrika we hapo upo, Kiswahilisasa kipo,
Kiswahili hazinetu, Afrika maendeleo.

7) Kwao i Pilipili, Kiswahili ya maboyi,
Afrika kwao ni asili, lugha yao ni mayayi,
Uzungu ni yao hali, Ulaya kwao uhayi,
Kiswahili hazinetu, Afrika maendeleo.

 8) Mwacha mila ndiye mtumwa, anakienzi utumwa,
Ustaarabu wa kutumwa, tayari wamechumwa,
Tayari wewe waumwa, wangoja tu kusukumwa,
Kiswahili hazinetu, Afrika maendeleo.